Friday 20 September 2013

LADY JAY DEE NA MIKE ROSS WATARAJIA KUFANYA SHOW KATIKA MISS TANZANIA-2013


Zikiwa zimebaki siku tatu kufanyika kwa fainali za mashindano ya Miss Tanzania, msanii mahiri kutoka Uganda Mike Ross na mwanamuziki wa hapa nchini Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ wanatarajiwa kutumbuiza katika fainali hizo Septemba 20 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na vyombo vya habari jana Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original, Victoria Kimaro alisema, burudani katika shindano hilo inatarajiwa kutolewa na wasanii hao wawili sambamba na kundi la Mama Afrika katika kukonga nyoyo za mashabiki watakaojitokeza ukumbini hapo.
“Tunaamini wasanii hawa watakonga nyoyo za mashabiki wa tasnia ya urembo hapa nchini, hivyo napenda kutoa wito kwa mashabiki kujinunulia tiketi mapema ili kuepuka usumbufu,” alisema Victoria. Naye Lady Jadee alisema, kwa kushirikiana na bendi yake ya Machozi wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa burudani ya nguvu kwa mashabiki wote watakaohudhuria.
“Nawaomba mashabiki wangu na wale wa urembo kujitokeza kwa wingi ili kufurahia burudani nzuri kutoka kwangu na bendi yangu ya Machozi, pia wasanii wenzangu waalikwa naamini watafanya vizuri siku hiyo,” alisema.
Kimaro alitangaza viingilio kwa ajili ya shindano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania wengi “kiingilio cha juu katika shindano hilo linalotarajiwa kufanyika keshokutwa (Jumamosi) katika Ukumbi wa Mlimani City ni Sh100,000 kwa viti maalumu, huku viti vya kawaida vikiwa Sh 50,000.”
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashimu Lundenga ambao ni waratibu wa Redd’s Miss Tanzania alisema, tiketi za shindano hilo tayari zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Alitaja maeneo ambayo yameteuliwa kuuza tiketi za Redd’s Miss Tanzania kwa mwaka huu ni duka la Shear Illusion lililopo Mlimani City, City Sports Lounge na Steers zilizopo Mtaa wa Samora, Faberk Fashion, Rose Garden Pub na ofisi za Redd’s Miss Tanzania ambazo zote zipo eneo la Mikocheni.
“Kwa mara nyingine tena napenda kuwashukuru wadhamini wetu wakuu  kinywaji cha Redd’s Original na wadhamini wenza ambao kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa zuri na lenye tija kubwa.”
Lundenga alifafanua kuwa ili kuwapa fursa watu wengi zaidi tiketi itakayonunuliwa katika vituo vilivyopangwa kabla ya shindano itakuwa ni Sh 80,000 na kutakuwa na ofa kadhaa.
Warembo watano waliofanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali ya Redd’s Miss Tanzania 2013  ni Miss Tanzania Photogenic 2013, Happiness Watimanywa.
Warembo wengine wanaowania nafasi hiyo ni Miss Tanzania Talent 2013, Prisca Clement, Miss Tanzania Personality, Severina Lwinga, Miss Tanzania Top Model 2013, Narietha Boniface na Miss Tanzania Sports Woman, Clara Bayo.
Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred, aliyefanikiwa kulitwaa mwishoni mwa mwaka jana.