Saturday 3 August 2013

HATMA YA USAJILI WA MRISHO NGASA ITAJULIKANA AUGUST 14

HATMA ya usajili wenye utata unaomhusu kiungo mshambuliji wa zamani wa Simba na Azam, Mrisho Ngassa, itajulikana Agosti 14, baada ya Kamati ya
Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kukaa na kupitia zoezi zima la usajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwanasheria, Alex Mgongolwa, inatarajiwa kuketi Agosti 13 na 14, kupitia pingamizi mbalimbali zitakazokatwa na klabu hizo kuhusiana na dosari na matatizo yaliyojitokeza, katika masuala ya uhamisho wa wachezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah, alisema pingamizi za usajili huo zitaanza kuwasilishwa rasmi kuanzia Agosti 6 hadi 12, mwaka huu.

“Masuala yote yanayohusiana na jinsi usajili ulivyokwenda, yanatarajiwa kujulikana baada ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kukaa na kupitia usajili huo, baada ya zoezi la pingamizi kwisha,” alisema Osiah.

Hivi karibuni baada ya Yanga kumaliza taratibu nzima za usajili wa mchezaji Mrisho Ngassa, anayedaiwa kumaliza mkataba wa mkopo wa kuitumikia Simba, akitokea Azam, kuliibuka taarifa kwa upande wa Simba zinazodai kuwa waliingia mkataba na mchezaji huyo.

Walisema kuwa mkataba huo wameshauwasilisha TFF, huku wakiiambia Yanga ‘imekula kwao’ na watakutana TFF kujua nani mwenye uhalali na mkataba wa mchezaji huyo.



Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...