Friday 2 August 2013

Ngassa, Chuji, Yondan, Cannavaro wakumbwa na balaa la kukatwa mshahara.

WACHEZAJI wanne wa klabu ya Yanga, wanatarajiwa kukatwa mishahara kutokana na kushindwa kuonyesha nidhamu nzuri na kudharau matakwa ya
mwalimu wa timu hiyo, Ernest Brandts.

Chanzo kimoja kilisema kuwa Tabia za wachezaji hao zimeuchosha uongozi na sasa kinachofuata ni kukatwa mishahara kwa kila mchezaji anayeonyesha utovu wa nidhamu kwa klabu na timu kiujumla.

Chanzo hicho kiliwataja wachezaji hao kuwa ni Mrisho Ngassa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Idd ‘Chuji’ na Kelivin Yondani, ambao walikuwa katika kikosi cha timu ya Taifa, kilichorudi nchini mwanzoni mwa wiki hii.

“Wachezaji hawa walipewa ruhusa ya kupumzika siku mbili, huku mwalimu akiwataka waripoti mazoezini leo (jana), lakini jambo la kushangaza hakuna hata mmoja wao aliyeweza kufika,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilieleza, wachezaji hao hawana sababu ambazo zimewazuia kufika mazoezini, kwani wangetakiwa kupiga simu na kueleza kilichowazuia kujiunga na wenzao kama walivyotakiwa na mwalimu.

“Tumesikia Ngassa yupo Mwanza, sawa haina tatizo, lakini wangetakiwa kusafiri ndani ya zile siku walizopewa na mwalimu, kipindi hiki ni kigumu katika maandalizi ya ligi, kwa kuwa ni mzunguko wa kwanza,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa hatua za kukatwa mishahara wachezaji hao, zitakuwa fundisho kwa wachezaji wengine, ambao wamekuwa wakijiamulia na kufanya mambo tofauti na mikataba yao waliyoingia na klabu hiyo.