Sunday, 13 October 2013

TRA yaanza kwa stail hii juu ya haki za kazi za wasanii wa muziki na filamu.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetangaza kuanza msako wa kukamata bidhaa za filamu na muziki
ambazo zinasambazwa nchini bila kubandika stempu za malipo ya kodi. Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi, Diana Masala, alisema Dar es Salaam jana kuwa msako huo utaanza rasmi Novemba Mosi, mwaka huu.

Alisema lengo ni kuhakikisha wasanii hawaibiwi kazi zao na wanapata faida kulingana na kazi zao.

Alisema kutokana na wizi wa kazi za wasanii, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Bodi ya Filamu Tanzania na wadau wengine wa filamu, walikubaliana kuanzisha utaratibu huo kwa lengo la kuwasaidia wasanii.

“Kuna watu wanatumia kazi za wasanii bila ya manufaa yoyote kwa wasanii wenyewe, hivyo tutakamata na kuharibu kazi hizo pamoja na kuwafungulia mashitaka wale wote tutakaowakamata,” alisema Masalla.

Ametoa wito kwa wasambazaji na waagizaji kupeleka maombi ya stempu za kodi kulingana na bidhaa zao, ili wapatiwe stempu hizo kwa ajili ya bidhaa zao.