Friday, 2 August 2013

Jay Dee kuvamia Arusha Idd Mosi

MSANII nyota wa muziki nchini, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ anatarajia kuvamia Mkoa wa Arusha kwa ajili ya kuitambulisha albamu yake mpya ya
‘Nothing But The Trust’ siku ya Iddi Mosi.

Katika ziara hiyo, Jay Dee anatarajia kuwa na bendi yake ya Machozi, huku akisindikizwa na Mwimbaji nyota wa muziki wa hip hop, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ katika maonyesho yatakayofanyika kwenye Ukumbi wa Triple A na Idd Pili kwenye Ukumbi wa Botanical Garden, ikiwa ni maalum kwa wanafamilia ambapo na watoto wataruhusiwa kuingia.

Akizungumza Dar es Salaam, Meneja wa Jay Dee, Gadna G Habash, alisema ziara hiyo ni mkakati uliokuwepo kwa muda mrefu kwa ajili ya kutoa burudani kwa mashabiki wao wa mikoani na kuwapelekea albamu mpya ya Nothing But The Trust iliyotoka hivi karibuni wakati wa kutimiza miaka 13.

“Tunatarajia kufanya ziara ya aina yake mkoani Arusha kwa ajili ya kuipeleka albamu mpya na pia Jay Dee hajafanya ziara mikoani kwa muda mrefu, hii ndio itakuwa fursa pekee kwa mashabiki wake, baada ya kumaliza Arusha atakwenda katika mikoa mingine,” alisema.