Friday, 2 August 2013

Yanga SC sasa yataka mazungumzo na Azam TV

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema upo tayari kukaa meza moja na Kampuni ya Azam, ili kukubaliana upya mapendekezo yao ya mechi zao kuonyeshwa
katika runinga yao. Uamuzi huo wa Yanga ulifikiwa jana katika kikao chao cha pamoja na viongozi wa klabu hiyo, sambamba na wenyeviti na makatibu wa matawi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Viongozi hao walianza kuunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ambao waliamua mechi zao zote za Ligi Kuu Bara ikiwa ni za nyumbani na ugenini zisionyeshwe katika runinga hiyo kutokana na kutoridhishwa na jinsi makubaliano hayo yalivyokwenda na Kamati ya Ligi.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake wa matawi, Bakieli Makele alisema msimamo wao ni huo huo, kwani klabu yao ni kubwa, hivyo haipaswi kutumiwa vibaya kwa ajili ya kuwanufaisha watu, lakini wapo radhi kukaa nao meza moja kwa ajili ya kulizungumzia hilo.

Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, kuwa wao wana mapendekezo yao ambayo hayakupewa nafasi kusikilizwa, hivyo kama uongozi wa Azam TV utakuwa radhi kukaa nao, wanaweza kuafikiana na kulimaliza suala hilo.